Tetesi zinaeleza kuwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamemalizana na beki wa kulia wa KMC FC, Israel Patrick Mwenda kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitatu kimya kimya na wanasubiri tu muda ufike ili wamtangaze.
Vinara hao wa ligi wamefanya usiri mkubwa juu ya usajili wa Mwenda sababu bado ana mkataba na KMC FC, ambao utamalizika mwisho wa msimu huu na wanaogopa yasiwatokee kama yale ya Edward Charles Manyama ambaye dili lake liliingiliwa na Azam FC wakambeba juu kwa juu.
Mwenda ni moja ya mabeki bora wa kulia nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga krosi za maana ambazo washambuliaji hufunga kwa urahisi, kukaba na kufunga mabao kutokana na mipira ya faulo kama ilivyokuwa katika mechi ya Taifa Stars dhidi ya Malawi.
Kusajiliwa kwa Mwenda maana yake Simba SC watakuwa na mabeki wa kulia watatu, Shomary Kapombe na ambaye ndio chaguo la kwanza, David Kameta ‘Duchu’ huku taarifa zinaeleza huenda akatolewa kwa mkopo kwani amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake.
Simba SC imejipanga kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji watakaoboresha kikosi chao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.