Uongozi wa Klabu ya Simba umetuma rasmi maombi kwenye klabu ya Al Hilal ya kutaka kuwasajili wachezaji wawili wa timu hiyo yenye maskani yake makuu katika mji wa Khartoum, Sudan.
Simba SC imetuma maombi ya kutaka kuwasajili Mlinda Lango wa timu hiyo, Issa Fontana, pamoja na mshambuliaji raia wa DRC Makabi Lilepo ambaye anatajwa kuja kuchukua nafasi ya Augustine Okrah ambaye amepewa mkono wa kwa heri baada ya msimu huu kumalizika.
Simba SC imetuma ombi la kumsajili Mlinda Lango Fontana kwa ajili ya kuziba nafasi ya kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manura ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa miezi minne akiuguza jeraha baada ya hivi karibuni kufanyiwa upasuaji wa nyama za paja.
Mmoja wa ‘Kigogo’ wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, amesema wanahitaji huduma ya wachezaji hao na tayari ofa iko mezani kwa vigogo hao wa Sudan.
Amesema wanaimani kubwa na kupata wachezaji hao kwa sababu ya ukaribu na urafiki uliopo kati ya Simba na klabu ya Al Hilal ambao wapo tayari kusikiliza ofa.
“Al Hilal wapo tayari kusikiliza ofa na kukaa meza moja kujadiliana kutokana na urafiki wa dhati uliopo kati yetu, kikubwa tunahitaji kuimarisha kikosi cha timu yetu kwa msimu ujao, tumedhamiria kufanya vizuri,” amesema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi.
Ameongeza kuwa wanaimani kubwa ya kupata huduma ya nyota hao kulingana na mahitaji ya timu yao kuelekea msimu ujao wa mashindano yatakayofanyika.
Aidha kwa upande wake, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kuhusu usajili msimu huu kila kitu kipo tayari na anaamini itakuwa na mwendo mzuri msimu ujao kwa kuwa inapata wachezaji wenye ubora kila idara.
“Kuhusu nani anasajiliwa hili jambo litawekwa wazi hapo baadaye na tayari kuna majina tunayo mezani kazi iliyopo ni mazungumzo, mashabiki wanapaswa kutulia na kujiandaa na msimu ujao kwani itakuwa timu kubwa na bora,” amesema Ahmed Ally
Simba SC kwa sasa inafanya maandalizi kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex Juni 6.