Klabu za Simba SC na Young Afrcans zimendelea kutajwa kama washindani wa kweli kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, kufuatia usajili na maandalizi wanayoyafanya kuelekea msimu mpya.
Klabu hizo kongwe katika ukanda wa Afrika mashariki na kati mara zote zimekua zikionekana kama taswira ya soka la Tanzania, kutokana na utayari wa kupambana kwenye michuano ya ndani na nje ya Tanzania.
Kocha mzawa Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema kwa mwonekano wa vikosi vya klabu za Simba SC na Young Africans unatoa taswira ya mchuano mkali katika kuwania taji la Ligi Kuu msimu huu, hasa baada ya upande mmoja kutwaa taji hilo mara tatu mfululizo tangu msimu wa 2017/18 hadi 2019/20.
Julio amesema aliona wachezaji wa Simba walivyocheza siku ya tamasha lao la Simba Day dhidi ya Vital’O ya Burundi na kila mmoja alipambana kumshawishi kocha ili kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
“Unamwona mtu kama Larry Bwalya anavyoonyesha uwezo licha ya ugeni alionao, naamini atasaidia sana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema jambo kubwa wanalopaswa kutambua wachezaji wa timu hiyo ni kutoridhika na mafanikio ya msimu uliopita.
“Yaani mataji ya msimu uliopita, wayasahau waanze kufikiria yaliyopo mbele yao, ili waendelee kufanya vitu vya tofauti katika kizazi chao.
Pamoja na Young Africans ilikuwa na changamoto ya kukosa kocha mkuu mapema, ilicheza vizuri dhidi ya Aigle Noir, hii inaonyesha msimu huu itakuwa na jipya kwa mashabiki wao, ambao walitamani kuona wachezaji wanaojituma ama wanaoweza kuwapa matokeo,” amesema.
“Klabu hizi zimejiwekea heshima nje ya mipaka yake, lakini haimanishi timu nyingine ni rahisi, bali kongwe zinatakiwa kuwa kioo cha kusajili vizuri na kuonyesha uwezo uwanjani,” amesema Julio akizungumzia msimu mpya unaoanza mwishoni mwa juma hili.
Young Africans wataanzia Dar es salaam wakiwakaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Mkapa na Simba watakuwa jijini Mbeya kwenye dimba la kubukumbu ya Sokoine, wakikaribishwa na Ihefu FC.