Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umeibuka na kutoa kauli kuhusu uwezekano wa Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama kurejea nchini na kuwatumikia Young Africans.
Simba SC wametoa kauli hiyo kufuatia Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mbata kuthibitisha kuwasiliana na RS Berkane ya Morocco kuangalia uwezekano wa kumsainisha Clatous Chama.
Mmoja wa viongozi wa Simba SC ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani amesema Young Africans wanajifurahisha kwani kwa mujibu wa makubaliano ya Mnyama na RS Berkane, Chama hawezi kuuzwa popote ndani ya miaka mitano ijayo bila Simba SC kuhusishwa.
Amedai kuwa kama wao watakuwa hawamuhitaji Chama ndipo watawaruhusu RS Berkane kumuuza popote, lakini si ndani ya ardhi ya Tanzania. Lakini rekodi zinaonyesha ni ngumu watani hao wa jadi kuuziana staa kama huyo.
Alipokua akizungumzia uwezekano wa kumsajili chama na kurejesha nchini Tanzania, Kaimu Ofisa Mtedani Mkuu wa Young Africans Senzo Mbatha alisema: “Chama ni mchezaji bora hakuna klabu ambayo itakataa kuwa naye na kwa sasa tunaiheshimu RS Berkane kwa kuwa bado wana mkataba naye lakini ni kweli tumeulizia uwezekano wa kumpata na kama kutakuwa na uwezekano wa kumleta hapa tutamleta.”
Senzo alisema hata hivyo Young Africans ya sasa haiko katika unyonge wa kumkosa staa yoyote ambaye wanamtaka hasa akipendekezwa na benchi lao la ufundi au kamati ya usajili.