Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, wamewasili jijini Arusha tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 11 wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union.
Simba SC watakua ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambao unatumiwa kwa muda na Coastal Union kama uwanja wao wa nyumbani kufuatia Uwanja wa CCM Mkwakwani kufungiwa na Bodi Ligi, kwa kupoteza sifa za kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu.
Kikosi cha Simba SC, kilichoko chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck na msaidizi wake Suleiman Matola, kiliwasili jijini Arusha jana jioni, kwa usafiri wa ndege kikipitia Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kiungo kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, ni miongoni mwa wachezaji wa Simba waliosafiri kuelekea jijini humo kwa ajili ya mchezo huo wa Novemba 21.
Morrison alikuwa nje kutumikia adhabu ya kukosa michezo mitatu pamoja na faini ya shilingi laki tano (500,000), baada ya kumpiga ngumi beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso wakati wa mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Uhuru wakati Simba ikichezeshwa mpira gwaride na kufungwa bao moja kwa sifuri.
Kiungo huyo alikosa michezo ya Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC ambapo Simba ilishinda kwa mabao matano kwa sifuri, dhidi ya Kagera Sugar, Simba ikishinda mabao mawili kwa sifuri na kisha mpambano wa dabi dhidi ya Young Africans uliokamilika kwa sare ya kufungana bao moja kwa moja.