Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene amewataka wafanyabiashara wa soko dogo la Kariakoo wanaojihusisha na usambazaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki laini yenye rangi nyeupe inayotumika kama kifungashio amewapa siku 14 kuiondoa sokoni mifuko hiyo.
Ameyasema jijini Dar es salaam mara baada ya kufanya ziara katika soko hilo na kubaini uwepo wa mifuko hiyo kinyume cha utaratibu.
Katika ziara hiyo, Simbachawene aliambatana na maofisa wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), amejionea namna mifuko hiyo iliyopigwa marufuku ikitumika kama kifungashio cha bidhaa za nyanya, karoti, vitunguu ambavyo vinaweza vikabebwa kwenye mifuko mbadala.
Aidha, Juni Mosi 2019, katazo la marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki lilianza kutumika rasmi, hata hivyo bado kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wamiliki wa viwanda vya plastiki kuendelea kutengeneza mifuko hiyo kinyume cha taratibu na sheria.
“Kwani mmelazimishwa kununua mifuko hii kiwandani, kwa nini msichukue mifuko mbadala na kuiuza? Kuna vikapu, mifuko ya karatasi kwa nini msichukue hiyo,” amehoji Simbachawene
“Watumiaji elimu imeshawafikia lakini nyie bado mnaendelea kuiuza. Kitendo cha mifuko hii kuendelea kuwepo sokoni kinawavunja moyo watengenezaji na wazalishaji wa mifuko mbadala.”amesisitiza
Hata hivyo, Simbachawene amesema kuwa taarifa alizonazo kuna viwanda vinne vya plastiki vinavyojishughulisha na uzalishaji wa mifuko hiyo laini iliyopigwa marufuku na Serikali huku akiwaagiza NENC kuvifuatilia mara moja.
Mjumbe wa bodi ya wafanyabiashara wadogo wa soko hilo, Rajabu Ally amedai kuwa wao hawana kosa bali wenye matatizo ni wenye viwanda vinavyozalisha mifuko hiyo.