Rais wa Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Said Naciri, ameahidi kutoa zaidi ya Shilingi za kitanzania milioni 18, kama bonasi kwa kila mchezaji, iwapo watafanikiwa kuifunga Kaizer Chiefs na kufuzu kwenda hatua ya fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Ahadi hiyo kwa wachezaji wa Wydad Casablanca imetoka, kufuatia changamoto inayowakabili ya kusaka matokeo ugenini Afrika Kusini dhidi ya wenyeji wao Kaizer Chiefs.
Mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika mjini Cansablanca mwishonij mwa juma lililopita, klabu hiyo anayoitumikia Mtanzania Simon Msuva, ilikubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Bao la Kaizer Chiefs kwenye mchezo huo ambao haukuhudhuriwa na mashabiki, lilifungwa na Mshambuliaji wao kutoka nchini Serbia Samir Nurkovic, katika kipindi cha kwanza.
Wydad Casablanca wanapaswa kusaka ushindi wa mabo mawili kwa sifuri na kuendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza mchezo wa Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, mwezi ujao.
Mchezo wa Fainali msimu huu 2020/21, umepangwa kuchezwa kwenye uwanja wa Mfalme Mohamed V, unaotumiwa na Wydad Casablanca, kama uwanja wao wa nyumbani, hivyo endapo watafaulu kutinga fainali watakua na faida ya kucheza nyumbani dhidi ya mshindi wa Nusu Fainali nyingine kati ya Al Ahly dhidi ya Espirace de Tunis.
Katika mchezo wa mkondo wa kwanza, Al Ahly iliibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri mjini Tunis, na mchezo wa mkondo wa pili utakaochezwa keshokutwa Jumamosi (Juni 26), utakua mjini Cairo kwenye uwanja wa Aslaam.