Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla amewataka Wakazi wa mkoa huo kuchukua tahadhari dhidi ya wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona, kwa kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara.

Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es salaam, RC Makalla amesema kuwa kutokana na jiografia ya Mkoa kuwa nyeti na unapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari zakutosha kwa kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara.

“Naomba tuchukue tahadhari moja ni kuvaa kwa usahihi barakoa kila wakati katika sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi kama kwenye vyombo vya usafiri, masoko, sherehe, nyumba za ibada, vituo vya afya na maofisini,” Amesema RC Makalla.

Tahadhari hii inakuja kufuatia taarifa kutoka Wizara ya Afya, juu ya uwezekano wa kutokea kwa wimbi la maambukizi ya Covid-19 ambayo yanakabili nchi nyingine hivyo kutahadhirisha umma kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia taarifa zinazotolewa.

Halikadhalika ameyataja makundi ya watu ambayo yapo hatarini kupata maambukizi ya corona kuwa ni wazee na watu wenye magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari, figo, kifua kikuu na magonjwa ya moyo.

RC Makalla Mkuu amewaagiza wakuu wa Wilaya zilizopo mkoani humo, Wakuu wa taasisi za Serikali na binafsi na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kusimamia maelekezo hayo.

Simon Msuva kulamba Milioni 18
Zaydi, Niyonzima kuikosa Simba SC Jumamosi