Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu ya Singida Big Stars imetoa taarifa za Kiungo Mshambuliaji Deus Kaseke kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Singida Big Stars itacheza dhidi ya Simba SC Ijumaa (Februari 03) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, mishale ya saa moja usiku.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu hiyo ya mkoani Singida Hussein Massanza amesema, kikosi chao tayari kimeshawasili jijini Dar es salaam, na kipo kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa Simba SC.
Amesema Kaseke hakuwa sehemu ya safari na kikosi chao, kutokana na adhabu iliyotangazwa dhidi yake ya kukosa michezo mitatu, kufuatia kosa la kujihusisha na imani za kishirikina.
“Timu imeshawasili Dar es salaam tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Simba SC, tutamkosa mchezaji wetu Deus Kaseke anayetumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu.”
“Tulianza kuikosa huduma yake katika mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Ruvu Shooting na sasa anaendelea kutumikia adhabu yake kwa kukosa michezo mingine miwili.”
“Kwa hiyo tutamkosa kwenye mchezo wetu na Simba SC na kisha tutaendelea kumkosa kwenye mchezo wetu mwingine dhidi ya Ihefu FC tutakaocheza Februari 12.”
“Hii haitupi shida, kwa sababu Singida Big Stars tuna kikosi kipana na chenye ubora mkubwa, tunaamini tutacheza dhidi ya Simba SC na kupata matokeo mazuri bila Kaseke.” amesema Massanza
Mchezo wa Duru la Kwanza uliopigwa Uwanja wa Liti mjini Singida dhidi ya Simba SC, Deus Kaseke aliifungia Singida Big Stars bao la kuongoza, kabla ya Peter Banda hajafunga bao la kusawazisha upande wa Mnyama.