Klabu ya Singida Big Stars imetamba kulipa kisasi dhidi ya Coastal Union katika mchezo wa Mzunguuko wa 25 wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa keshokutwa Jumapili (Machi 12), kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Singida Big Stars imetamba kufanya hivyo, huku ikikumbuka kupoteza mchezo wa Duru la Kwanza uliowakutanisha na Wagosi wa Kaya mjini Singida katika Uwanja wa CCM Liti tarehe 07/12/2022, kwa kufungwa 2-1.
Afisa Habari wa Singida Big Stars, Hussein Massanza amesema wamejiapnga vizuri kuhakikisha Kisasi hicho kinalipwa, kwani wana kikosi bora na imara ambacho kinaweza kufanya maajabu katika uwanja wa ugenini.
“Kumbukumbu mbaya kwetu ilikuwa tulipopoteza kwa mabao 1-2 kwenye uwanja wa nyumbani CCM Liti dhidi ya Coastal Union.”
“Mpaka sasa, Coastal Union ndio timu pekee iliyofanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwenye uwanja wetu wa CCM Liti.”
“Hivyo na sisi tumejiandaa vema kuhakikisha tunalipa kisasi kwa kupata alama tatu katika uwanja wao wa nyumbani kama walivyotufanyia sisi.”
“Maandalizi tumeshaanza kwa ajili ya mchezo huo na tunaenda kulipa kisasi baada ya mzunguko wa kwanza kupokea kipigo.”
“Timu yetu inajiandaa vizuri kwa ajili ya kupambana kwenye mchezo huo, tutapambana kwa ajili ya kupata pointi tatu ili kuwa kwenye nafasi nzuri.”
“Tutaingia kwa tahadhari kubwa na kuwaheshimu wapinzani wetu, tutapambana sana maana kila timu inapambana kupata matokeo iwe nyumbani au ugenini.”
Singida Big Stars ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya alama 47, wakati Coastal Union ikiwa na alama 24, nafasi ya 11, zote zimecheza michezo 24.