Klabu ya Singida Big Stars rasmi imesitisha mbio za ubingwa Tanzania Bara, baada ya kukiri mambo yamekua magumu na haitaweza kuingia anga za Simba SC na Young Africans.
Singida Big Stars inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza, ipo nafasi ya nne katika msimamo ikiwa na alama 43, sawa na Azam FC inayobebwa na uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kocha msaidizi wa Klabu hiyo ya mkoani Singida Mathias Lule amesema, hadi sasa wanashukuru kwa kazi kubwa iliyofanywa na kikosi chao, na imedhihirika wana kikosi cha aina gani katika Michuano ya Ligi Kuu.
Kocha huyo kutoka nchini Uganda amesema, inashangaza kuona Klabu inayoshiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kuwa na kiwango kikubwa kama Singida Big Stars, hivyo hawana budi kumshukuru mungu kwa hatua hilo.
Kuhusu Ubingwa, Kocha huyo wa zamani wa klabu Mbeya City amesema ni dhahir wameshaondoka katika mbio za Ubingwa, na wanachokifanya sasa ni kuhakikisha wanamaliza katika nafasi nzuri ili wapate nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao.
“Tunashukuru kuona timu imekua na muendelezo mzuri, licha ya ugumu na ugeni wetu katika Ligi Kuu msimu huu, kuhusiana na ubingwa ukweli ni kwamba hatuna mpango wa kupambania kuwa kinara wa msimamo.”
“Kwa sasa mawazo yetu yote yapo katika kuhakikisha tunakuwa na mwendelezo wa matokeo mazuri, ili kumaliza kwenye nafasi nzuri na ikiwezekana tucheze Michuano ya Kimataifa msimu ujao.” amesema Kocha Lule
Singida Big Stars kwa sasa inajiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ihefu FC itakayokuwa nyumbani Wilayani Mbarali mkoani Mbeya katika Uwanja wa Highland Estate.