Kikosi cha Azam FC kimeanza mawindo ya mchezo wa Mzunguuko wa 23 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, utakaoapigwa Februari 21, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo Azam FC itakua mgeni wa Simba SC, huku ikiwa na deni la kulinda heshima ya ushindi iliyoupata kwenye Duru la Kwanza la Ligi Kuu, ikichomoza na ushindi wa 1-0, bao likifungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Dube.

Katika kuhakikisha mpango wa kutunza heshima mbele ya Simba SC msimu huu 2022/23 unatimia Februari 21, Azam FC itajiandaa kwa kucheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya KMKM inayoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye Kurasa za Mitandao ya Kijamii za Azam FC, Mchezo huo umepangwa kupigwa kesho Jumamosi (Februari 11) jijini Dar es salaam.

“Katika kuwaweka kwenye ushindani wachezaji wetu na kujiandaa na mechi za mashindano, kikosi chetu kimatarajia kucheza mchezo wa kirafiki dhidi KMKM utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Jumamosi saa 1.00 usiku.” imeeleza taarifa ya Azam FC

Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kucheza michezo 22, Azam FC inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 43 sawa na Singida Big Stars inayoshika nafasi ya nne.

Simba SC ipo nafasi ya pili kwa kufikisha alama 53, ikitanguliwa na Young Africans iliyo kileleni kwa tofauti ya alama sita.

Tetemeko Syria, Uturuki: Vifo vyafikia 20,000
TCRA yaongeza uthibiti picha zisizofaa: Nape