Bilionea Sir Jim Ratcliffe anataka kuweka ofa nyingine ya kununụa hisa za klabu ya Manchester United baada ya juhudi za kuimiliki klabu hiyo jumla kugonga mwamba.
Mwekezaji huyo kutoka England alichuana vikali na Bilionea mwingine kutoka Qatar Sheikh Jassim katika kinyang’anyiro cha kununua klabu hiyo inayomilikiwa na familia ya Glazers.
Licha ya wamiliki wa sasa kuiweka sokoni Man United tangu Novemba mwaka jana (2022), dili limekwama na majidiliano kati ya wawekezaji hao bado hayaeleweki.
Taarifa zimeripoti kwamba makubalino hayakufikiwa kati ya wawekezaji hao kuhusu mauzo ya klabu ambayo inatajwa kuwa inauzwa kwa Pauni 6 Bilioni.
Ratcliffe alipendekeza kuweka ofa ya Pauni 5 Bilioni mapema mwaka huu, sambamba na Sheikh Jassim lakini ofa hiyo haijawaridhisha na mabosi wa klabu.
Hivyo mwekezaji huyo mwenye umri wa miaka 70 anayemiliki kampuni ya Ineos amepanga kununua sehemu ndogo tu ya hisa za klabu hiyo, kwa mujibu wa ripoti.
Chanzo cha habari kimeripoti kwamba mwekezaji huyo huenda akanunua asilimia 25 tu ya hisa za klabu ya Man United zenye thamani ya Pauni 1.5 Bilioni.
Kwa hiyo hisa hizo zitagawanywa mara mbili (A na B), hisa za kwanza (A) zitamilikiwa na Ratcliffe, hisa za pili (B) atabaki nazo familia ya Glazers.
Iwapo pendekezo la Ratcliffe litakubaliwa, ina maana kwamba wamiliki wa Marekani wataendelea kuwa na udhibiti wa klabu.
Hata hivyo, uamuzi wa Ratcliffe hautawapendeza Mashabiki wa Man United pamoja na wachezaji wa zamani klabu hiyo ambao wanaipinga familia ya Glazers.
Hata hivyo, inaweza kuongeza mtaji wa ziada kwa ajili ya uhamisho au maboresho kufanywa katika Uwanja Old Trafford.
Wakati huo huo, Sheikh Jassim hajabadilisha malengo yake ya kuwa mmiliki mkuu wa klabu ya Man Utd.