Kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amewapa mtihani washambuliaji wa klabu hiyo, Alexis Sanchez na Romelu Lukaku akiwataka kujipandisha wenyewe.
Lukaku mwenye umri wa miaka 25 na Sanchez mwenye umri wa miaka 30 walikumbwa na joto la kukataliwa kimtindo na Jose Mourinho aliyekuwa anakiongoza kikosi cha wekundu hao wa Old Trafford kilichokumbwa na dhahma ya kuzamishwa chini ya nafasi tano za juu za Ligi Kuu ya Uingereza.
Mara ya mwisho, Sanchez alicheza dhidi ya Crystal Palace mwezi Novemba na hakuonekana tena uwanjani kutokana na kuwa majeruhi. Lukaku ambaye alimwaga wino kwa £75Milioni mwaka jana kujiunga na Man Utd, hajahusishwa kwenye michezo miwili ya awali chini ya utawala mpya wa Solskjaer.
Lukaku ameshaifungia Man Utd magoli 6 kwenye michezo 16 ya msimu wa Ligi huku Sanchez aliyejiunga na klabu hiyo Januari mwaka huu akitokea Arsenal akiwa amefunga goli moja kwenye michezo 10.
Kwa mujibu wa Solskjaer, wachezaji hao wamerejea mazoezini wakijifua kwa ajili ya michezo inayofuata ikiwa ni pamoja na mchezo wa kesho dhidi ya Bournemouth, hivyo amewapa mtihani wa kumshawishi.
“Lukaku, Martial na Sanchez walikuwa kwenye mazoezi jana na natumaini wanaweza kujiunga na mazoezi ya leo. Ngoja tuone namna ambavyo watatuonesha utayari wao,” alisema Solskjaer.
“Kazi yangu mimi ni kuwapa maelekezo na wao wajibu wao ni kuyafanyia kazi. Niko hapa kuwaweka kwenye njia sahihi na wao ni uamuzi wao kuendelea kupita kwenye njia hiyo, huo ndio msingi wa mpira wa miguu,” aliongeza.
Kocha huyo ambaye ameingia na baraka za ushindi alieleza kuwa wachezaji hao wanapaswa kufanya alichokifanya Paul Pogba kwa kujipandisha akiifungia klabu hiyo magoli mawili dhidi ya Huddersfield, Jumatano na kufanikisha ushindi wa 3-1.
Man Utd inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 32, takribani alama 19 nyuma ya Liverpool iliyoko kileleni.