Meneja wa muda wa Klabu ya Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer ameweka wazi mtihani aliopewa na Bodi ya timu hiyo punde alipokabidhiwa kikosi hicho kilichokuwa kimeanza kupoteana katika kipindi cha mwisho cha uongozi wa Jose Mourinho.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Solskjaer amesema kuwa mwajiri wake huyo alimpa vipengele vitatu kwenye mtihani huo, ambavyo ni kuhakikisha anarudisha morali wa wachezaji, kuongeza kiwango cha uchezaji na kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Kocha huyo alikabidhiwa kikosi cha Wekundu hao wa Old Trafford Desemba mwaka jana baada ya Jose Mourinho kutimuliwa. Hadi sasa, Solskjaer ameshafanikiwa kushinda mechi tisa kati ya 10.
Vivyo hivyo, katika kipengele cha pili cha mtihani wake anaonekana kufanya vizuri kwa kuzingatia kuwa Paul Pogba, Marcus Rashford na Anthony Martial wanaonekana kurejea klabuni hapo kiakili na kufanya kweli.
Kutokana na mafanikio hayo, kocha huyo aliyewahi kuitumikia klabu hiyo na kuacha historia nzuri, anatabiriwa mazuri na wengi kuwa ataweza kukabidhiwa timu hiyo kwa mkataba rasmi. United wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi akiwa na alama 48.