Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameitaka Serikali kueleza kwa nini ujenzi wa mradi wa Bandari ya Bagamoyo mkoani Pwani haujengwi licha ya mzabuni kupatikana kutoka nchini China.
Spika Ndugai amesema hayo leo Jumatatu Mei 13, 2019 bungeni baada ya wabunge mbalimbali kuhoji mradi huo wa bandari kukwama wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya wizara ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano ya mwaka 2019/20 ya Sh4.9 trilioni.
Spika Ndugai amesema ujenzi wa bandari hiyo ukikamilika utakuwa na tija kubwa kwa nchi kuliko ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaojengwa, “Yaani bora tungeanza na bandari hii ya kisasa kabisa tukaja reli.”
Amesema kukamilika kwa reli ya SGR bila kuwa na bandari ya kisasa kama hiyo ambayo ilikuwa ijengwe Bagamoyo ni kazi bure kwani mpaka sasa nchini hakuna bandari nzuri hivyo Serikali inapaswa kuliona hili.
Amemtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe pindi atakapokuwa akihitimisha mjadala wa bajeti yake leo Jioni kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
Wakati Spika akitoa maelekezo hayo, wabunge wa pande zote walikuwa wakimshangilia.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengelwa amemuomba Spika Ndugai kuunda kamati ya kwenda kuchunguza suala la ujenzi wa bandari hiyo ili ukweli wa mkwamo huo uweze kujulikana na kuishauri vyema Serikali.
Baadhi ya wabunge wengine ambao wamehoji bandari hiyo kutojengwa na wakihitaji ufafanuzi ni Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM), Lucy Magereli (Viti Maalum-Chadema), Ally Salehe (Malindi-CUF), Charles Tizeba (Buchosa-CCM) na Dk Shukuru Kawambwa (Bagamoyo-CCM).