Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa atahakikisha Chama cha Demokrasia na Maendeleoa kinapata haki yake ya nafasi ya ubunge wa bunge la Afrika Mashariki kwani haki yao.
Amesema kuwa hadi sasa nafasi hizo bado ni za Chadema na atahakikisha haki hiyo wanaipata endapo tu watafuata kanuni na taratibu za kuwapata wagombea wa nafasi hizo na kwamba Katibu wa Bunge atatoa taarifa ni lini mchakato huo utafanyika.
Aidha, Ndugai ametoa tahadhari kwa chama hicho kuwa yeye ndiye mwenye Mamlaka ya kutoa utaratibu wa kupatikana kwa wawakilishi wa Tanzania kupitia vyama vya upinzani, hivyo endapo wasipotumia nafasi hiyo, atatumia mamlaka aliyonayo kutangaza utaratibu mwingine ili Tanzania isikose wawakilishi katika nafasi hizo.
“Ikumbukwe kuwa maamuzi haya ya kuwatenganisha wabunge wa upinzani kwa kuangalia vyama vyao ni maamuzi ya Spika, tukumbuke mabunge yaliyopita maspika wenzangu hawakufanya hivyo, waliwaweka wabunge wote wa upinzani kwenye kundi moja, mimi nikasema twende na demokrasia hii ya wawili”, Amesema Ndugai
Hata hivyo, uchaguzi uliofanyika juzi, Bunge hilo liliwachagua wajumbe 7 kati ya 9 waliohitajika huku wagombea wawili wa Chadema wakienguliwa kwa kura za hapana.