Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amepiga marufuku wabunge kufanya vituko mbalimbali ikiwemo kuruka sarakasi, kupiga magoti, na kuja na vilevi wakati wakichangia mijadala mbalimbali ndani ya bunge.
Dr. Tulia ametoa maelekezo hayo Mei 24, 2022 baada ya Mbunge wa Igalula Venant Daud Protas kuomba mwongozo wa Spika baada ya kutokea vituko kadhaa bungeni siku mbili mfululizo.
Mheshimiwa Protas alitaka kujua kama Bunge linaruhusu Wabunge kuchangia mijadala kwa kufanya vituko ndani ya bunge na Spika akamjibu kwa kukataza matendo hayo.
“Hairuhusiwi na nimeshatoa maelekezo asitokee mtu humu ndani kuchangia hoja kwa kufanya kituko hairuhusiwi kupiga sarakasi humu ndani na asije mwingine akafanya jambo linaloashiria anachangia kwa kufanya mambo kama hayo,” amefafanua Dkt. Tulia.
Hapo jana mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay alipanda juu ya meza na kupiga sarakasi wakati akichangia hoja ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ndani ya bunge May 23, 2022 na kutaka kupewa majibu ya lini barabara jimboni kwake zitatengenezwa.
Tukio jingine ni lile lililofanywa na Mbunge wa viti Maalumu Jacqueline Msongozi baada ya kupiga magoti bungeni wakati akichangia hoja yake May 24, 2022 na kutishia kuondoka na shilingi ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi endapo Waziri hatatolea maelezo ya ujenzi wa kivuko Mtomoni.
Mei 9, 2022 pia lilitokea tikio la Mbunge wa Momba (CCM), Condesta Sichalwe kuingia na pombe za kienyeji bungeni wakati akichangia hoja ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2022/2023 ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na biashara akitaka zipimwe kisha zirasimishwe.