Washambulaiji Wakongwe Luis Suarez na Edinson Cavani wamejumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uruguay itakayoshiriki Fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu 2022.
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Uruguay Diego Alonso, ametaja kikosi cha wachezaji 26, kitakachoanza safari ya kuelekea Qatar, tayari kwa Fainali hizo zitakazoanza Novemba 20.
Suarez ambaye aliwahi kucheza kwa mafanikio makubwa akiwa na klabu za Liverpool na FC Barcelona ametajwa kwenye kikosi cha Uruguay akiwa na umri wa miaka 35, sawa na mkongwe mwenzake Cavani, ambaye tayari ameshaifungia Valencia mabao manne msimu huu 2022/23.
Beki Mkongwe Diego Godin mwenye umri wa miaka 36, naye ametajwa kwenye kikosi cha Uruguay.
Wachezaji watatu wanaocheza Ligi kuu ya England (Premier League) Mshambuliaji wa Liverpool Darwin Nunez pamoja na Viungo Rodrigo Bentancur wa Tottenham na Facundo Pellistri wa Manchester United, nao watakwenda Qatar.
Uruguay imepangwa Kundi H, sambamba na timu za Mataifa ya Korea Kusini, Ureno na Ghana.
Kikosi kamili kilichotajwa leo Ijumaa (Novemba 11) na Kocha Mkuu Diego Alonso.
WALINDA LANGO: Fernando Muslera (Galatasaray), Sergio Rochet (Nacional), Sebastian Sosa (Independiente).
MABEKI: Jose Maria Gimenez (Atletico Madrid), Sebastian Coates (Sporting CP), Diego Godin (Velez Sarsfield), Martin Caceres (LA Galaxy), Ronald Araujo (Barcelona), Guillermo Varela (Flamengo), Jose Luis Rodriguez (Nacional), Mathias Olivera (Napoli) na Matias Vina (Roma).
VIUNGO: Lucas Torreira (Galatasaray), Manuel Ugarte (Sporting CP), Matias Vecino (Lazio), Rodrigo Bentancur (Tottenham Hotspur), Federico Valverde (Real Madrid), Facundo Pellistri (Manchester United) na Nicolas De La Cruz (River Plate).
WASHAMBULIAJI: Agustin Canobbio (Athletico Paranaense), Facundo Torres (Orlando City), Giorgian De Arrascaeta (Flamengo), Maxi Gomez (Trabzonspor), Luis Suarez (Nacional), Edinson Cavani (Valencia) na Darwin Nunez (Liverpool).