Serikali ya Sudan na viongozi wa makundi ya waasi leo wanatarajiwa kutia saini mkataba wa kihistoria wa amani unaonuia kumaliza miongo kadhaa ya vita iliyosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok, wakuu wa serikali ya mpito na viongozi wa makundi ya waasi kutoka majimbo ya Darfur, Kordofan ya Kusini na Blue Nile ndiyo watakaoongoza tukio hilo muhimu.
Halfa rasmi ya kutiwa saini mkataba huo inafanyika kwenye mji mkuu wa taifa jirani la Sudan Kusini, Juba na wawakilishi kutoka Misri, Qatar na Saudi Arabia wakiwa miongoni mwa wanaohudhuria.
Suala la kukomesha mizozo ya ndani nchini Sudan imekuwa kipaumble cha serikali ya mpito iliyoingia madarakani tangu kuangushwa kwa utawala wa Omar al-Bashir mwaka uliopita.