Zaidi ya watu Sabini wamefariki dunia kutokana na mafuriko yaliyoikumba nchi ya Sudan, na kusababisha uharibifu wa mali na nyumba kuzama.
Habari kutoka nchini humo zinaeleza kuwa hayo ni mafuriko mabaya zaidi kuwahi kuikumba Sudan, ambapo tayari nchi hiyo imeomba msaada wa kimataifa wa kukabiliana na idadi kubwa ya watu wanaohitaji misaada mbalimbali.
Serikali ya Sudan imesema imejaribu kusambaza misaada kadhaa kwa wahitaji lakini haitoshi, kwani wengi bado hawajafikiwa na misaada hiyo.
Baadhi ya watu walioyakimbia makazi yao baada ya nyumba zao kuharibiwa na mafuriko hayo wameilaumu Serikali kwa kushindwa kuwapatia misaada, na hivyo kufanya maisha yao kuwa hatarini.
Vijiji vipatavyo hamsini vimeharibiwa na mafuriko hayo yaliyoyakumba majimbo manane katika nchi hiyo ya Sudan.
Kingo za mto Nile wenye matawi yake nchini Sudan zimepasuka baada ya kuzidiwa na maji, ambapo maji hayo yamekuwa yakiingia kwenye makazi ya watu.