Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Sven Vandenbroeck amesema amekua akipata wakati mgumu, kufuatia baadhi ya wachezaji wake kumkasirikia kwa kufanya maamuzi ya kupanga kikosi kabla ya mchezo.
Kocha Sven amekua na maamuzi tofauti ya kupanga kikosi chake, kutokana na kuwa na wachezaji wenye uwezo unaoshabihiana kwa asilimia kubwa, lakini hupata changamoto, ambazo ameamua kuzianika hadharani.
Amesema amekuwa akitofautiana mara kadhaa na baadhi ya wachezaji kutokana na maamuzi yake juu ya wachezaji gani wanaopaswa kuanza na wale watakaokaa benchi kwenye michezo yao.
“Nina furaha na kila mchezaji anayeunda kikosi changu, hii inajumuisha hata wale ambao hawachezi mara kwa mara, kwa bahati mbaya kwenye kila mchezo ni wachezaji 18 pekee ambao wanakuwa kwenye listi na wachezaji wengine kumi hawapati kabisa nafasi ya kuwa sehemu ya mchezo.”
“Kuna wakati ninapofanya maamuzi ya wachezaji gani watacheza wapo baadhi ya nyota ambao hukasirishwa na hilo na mara kadhaa hubaki wakiwa na hasira kwa siku nzima lakini jambo zuri ni kuwa kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo ambavyo nao wanaelewa kuwa hali hii ni ya kawaida na ni lazima itokee.” amesema kocha Sven.
Simba imeshashuka dimbani mara tano msimu huu, na kocha Sven amebadilisha kikosi chake mara kadhaa, hali ambayo imemsaidia kuibuka na ushindi mara nne na kuambulia matokeo ya sare kwenye mchezo mmoja.
Michezo aliyoshinda ni dhidi ya Ihefu FC (2-1), Biashara United (4-0) , Gwambina FC (3-0), JKT Tanzania (4-0), huku Mtibwa Sugar wakigoma kutoa alama tatu kwa mabingwa hao mara tatu mfululizo kwa kulazimisha sare ya bao moja kwa moja.