Taasisi za sekta ya Afya na Vyuo vya Afya nchini vimetakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuboresha tiba asili ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukizwa.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Edward Mbaga alipokuwa akifungua kikao cha viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya na Vyuo vya Taaluma ya Afya nchini.
Kikao hicho kilikuwa na dhumuni la kuboresha ushirikiano na kuangalia namna ya kuongeza rasilimali katika kupanua zaidi tiba asili nchini.
Mbaga amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha utoaji huduma asili kwa kuhakikisha jamii inatumia dawa salama zenye ufanisi na ubora katika kulinda afya ya jamii kwa ujumla kwa kufanya tafiti za kina kwa dawa asilia.
Ameeleza kuwa serikali imetambua umuhimu wa tiba asili tangu mwaka 1969 na kuna zaidi ya miti ya 12,000 Tanzania ambayo inatibu magonjwa mbalimbali.