Baadhi ya Watu wenye afya bora ya akili wametajwa kuwa na uwezekano wa kuwa na magonjwa ya akili, na kwamba watu ambao hawana ugonjwa wa akili nao pia wanaweza kuwa na afya mbaya ya kiakili na hivyo kushauriwa kuwa makini na utaratibu wa maisha ili kuepukana na tatizo hilo.
Hayo yamebainishwa hii leo Novemba 13, 2022 na Mtaalamu wa masuala ya Afya, Dkt. Richard Kaniki wakati akifanya mahojiano na Dar24 na kuongeza kuwa, hali ya kutokuwa sawa kiakili na kisaikolojia au kutokuwepo kwa usumbufu wa akili ya mtu, ni dalili tosha za ugonjwa huo.
Amesema, “Mtu mwenye afya njema ya akili anakuwa na mawazo chanya, kuwa sawa kijamii na kisaikolojia na ana uwezo wa kuchangia katika utendaji wake wa kila siku na pia anakuwa na uwezo wa kuridhisha wa kimawazo na kitabia lakini ikiwa tofauti basi lipo tatizo.”
Dkt. Kaniki amefafanua kuwa, uwezo wa mtu kuwa timamu kiakili unahusisha uwezo wa kutatua matatizo mbalimbali yanayomkabili katika maisha ya kila siku yakihusisha msongo wa mawazo, shuguli za uzalishaji na mchango wake katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Aidha, mesema, “Kwanza ni vyema kutambua kwamba afya ya akili inahusisha ustawi wa akili, kujitambua kwa ufanisi, uhuru, umahiri, utegemezi na kujitambua kwa uwezo wa kiakili na kihemko kwa kujilinganisha wa watu wengine sasa kama unaona haupo katika kundi hili mtu ajijue ana shida.”
Hata hivyo, amesema ili kusaidia kutunza afya ya akili ni lazima mtu awe na mitazamo chanya kimaisha, kimaendeleo na watu au vitu vinavyomzunguka, kuwa na ushirikiano, kujitawala, kumudu mazingira yanayokuzunguka ikiwa ni pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na watu.