Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kuondoka kesho Jumamosi (Machi 13) kuelekea Nairobi, Kenya tayari kwa michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Harambee Stars’.
Taifa Stars imefanya mazoezi ya mwisho leo Ijumaa (Machi 12) asubuhi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kusafiri kesho Jumamosi mchana kwenda nchini Kenya.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kocha mkuu wa kikosi hicho Kim Poulsen ameeleza namna safari itakavyokuwa na maandalizi ya timu kwa ujumla kuelekea mechi hizo.
“Tutaondooa kesho mchana kwa ndege na tukifika Nairobi, Kenya tutaweka kambi ili kupata muda kidogo wa kupumzika kisha tuendelee na mazoezi wakati wa jioni,”
“Tutaondoka na wachezaji wote hawa mliowaona leo (22), pia Himid Mao ambaye amewasili nchini alfajiri ya leo.”
“Wachezaji wengine wale wa Simba na ambao hawajaripoti kambini watakuja moja kwa moja Kenya kuungana na timu kwaajili ya mechi zitakazofuata,” amesema Kim.
Taifa Stars itaitumia michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kenya kwa ajili ya kujiandaa na mtihani wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2021). Taifa Stars itacheza ugenini dhidi ya Equatorial Guinea (Machi 25) na kisha itarejea jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa kucheza dhidi ya Libya (Machi 28).
Wachezaji Taifa Stars walioitwa kwa ajili ya michezo hiyo ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika (AFCON 2021): Aishi Manula, Metacha Mnata, Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Israel Mwednwa, Erasto Nyoni, Dickson Job, Bakari Nondo Mwamnyeto, Kelvin Yondan, Carlos Protas, Laurent Alfred, Kennedy Juma, Mohammed Hussein, Nickson Kibabage na David Bryson.
Wengine ni Yassin Mustapha, Edward Manyama, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Mzamir Yassin, Jonas Mkude, Saidi Ndemla, Fiesal Salum, Himid Mao, Ally Msengi, Baraka Majogoro, Salum Aboubakar, Iddy Nado, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na John Bocco.
Pia wapo Yohanna Mkomba, Shaban Chilunda, Ditram Nchimbi, Deus Kaseke, Abdul Suleiman, Kelvin Pius John, Nassor Hamoud na Meshack Mwamito.