Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kitacheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki iliyo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la duniani FIFA, baadae mwezi huu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limethibitisha uwepo wa michezo hiyo miwili ya kimataifa ya kirafiki, ambapo kikosi cha Taifa Stars kitakachoitwa na kocha mkuu Shaban Salum Mayanga kitaanzia ugenini nchini Algeria Machi 22 dhidi ya wenyeji, kabla ya kurejea nyumbani Dar es Salaam kuwakali The Leopards (Timu ya taifa ya Jamuhuri Ya Kidemokrasia Ya Kongo) Machi 27 Uwanja wa Taifa.
Mara ya mwisho Taifa Stars iliteremka uwanjani Novemba 1 na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l’Amitie, au Urafiki mjini Cotonou.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa dakika ya 33 kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu na kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto dakika ya 50.
Matokeo haya yanamaanisha Benin ilishindwa kulipa kisasi kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.
Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 146 kwenye viwango vya FIFA, wakati DRC ni ya 39 na Algeria ni ya 60.