Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imekata tiketi ya kucheza Fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika nchini Ivory Coast mapema mwaka 2024.

Stars iliyokua inahitaji alama moja ili kufanikisha kukata tiketi ya kushiriki Fainali hizo, iliambulia matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Algeria iliyokua nyumbani.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwa timu hiyo inayonolewa na Kocha kutoka nchini Algeria Adel Amrouche, kwani iliwalazimu kucheza kwa kujihami zaidi, huku ikitumia nafasi chache kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hayakuleta madhara katika lango la wenyeji.

Kwa sare hiyo Stars inafikisha alama 08, ikitanguliwa na Algeria yenye alama 16, huku Uganda iliyokua nyumbani ikicheza dhidi ya Niger ikibaki nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 07.

Uganda ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 2-0 dhidi ya Niger lakini ushindi huo haujaisaidia lolote nchi hiyo kutoka Afrika Mashariki.

Hii inakuwa mara ya tatu kwa Taifa Stars kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ambapo kwa mara ya kwanza ilifanya hivyo mwaka 1980 katika Fainali zilizochezwa nchini Nigeria, kisha mwaka 2019 nchini Misri na sasa inakwenda Ivory Coast.

Gamondi: Hatutakuwa wanyonge ugenini
Hali ni tete: Mauaji ya kutisha Uraiani, Jeshini