Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa siku 14 kwa viongozi wa Mkoa wa Dar-es-salaam kuhakikisha kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi Luis kinaanza kutumika ifikapo Desema 20,2020.
Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho leo, Mhandisi Nyamhanga amewataka viongozi hao kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa maeneo yaliyobaki ili kuanza kutoa huduma za usafiri kwa jamii
Nyamhanga amesema kuwa kazi ya ujenzi wa kituo hicho imekamilika kama ilivyoelekezwa na Desemba 1, mwaka huu msimamizi wa ujenzi ambaye ni Chuo Kikuu cha Ardhi Dar-es-salaam, kilitoa hati ya awali ya kukamilika kwa ujenzi kwa mkandarasi ambapo sehemu kubwa imekamilika , hivyo kituo hicho kipo tayari kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji kwa jamii.
Aidha, ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar-Es-Salaam kwa kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo kwa weledi na kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati uliopangwa huku akitoa maelekezo kwa uongozi huo kuhakikisha maandalizi muhimu yanafanyika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika stendi hiyo ili kusiwepo na changamoto kituo hicho kitakapoanza kutumika.
Wakala wa Barabara TANROAD wameagizwa kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya kuingia kituoni hapo ili kuweza kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.
Vilevile, Mhandisi Nyamhanga ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuhakikisha wanaandaa mpango kabambe wa eneo lililopo karibu na stendi ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza kwenye ujenzi wa mahoteli na nyumba za kulala wageni ili kuwarahisishia wasafiri maeneo ya kufikia wanapokuwa safarini.