Katika kuelekea sikukuu ya Eid el-fitr, Jeshi la Polisi nchini limesema hali ya usalama ni shwari na kwamba litaendelea kusisitiza jamii kutoa ushirikiano katika kubaini na kuzuia uhalifu unaotokana na mmomonyoko wa maadili ambao unaoiandama dunia kwa sasa pamoja na ajali za barabarani
zinazosababisha vifo na majeruhi.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, David Misime imesema waislamu wiki hii watahitimisha ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na baada ya ibada watasheherekea katika maeneo mbalimbali baada ya baraza la Eid.
Amesema, Jeshi la Polisi nchini limejipanga kikamilifu kwa kushirikiana na viongozi wa dini ya kiislamu na wananchi kuhakikisha usalama unaimarishwa maeneo yote ili kutoa fursa ya kusheherekea kwa amani na utulifu, makamanda wa mikoa na vikosi watasimamia usalama kulingana na mazingira na mikoa na vikosi vyao.
Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda watoto ili wasipatwe na madhara ya aina yoyote wanapokuwa wakisheherekea sikukuu katika maeneo mbalimbali na siku kuu hiyo ya Eid el- fitr inatarajiwa kusheherekewa kesho au kesho kutwa (Aprili 21 au 22, 2023), kulingana na muandamo wa mwezi.