Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameagiza mikakati ya muda mfupi ifanyike kuboresha huduma katika kituo cha huduma kwa wateja cha Shirika la Umeme Tanzania – TANESCO, ambapo watu watatu pekee kati ya 10 ndio wanaweza kusikilizwa kwa siku.
Ametoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara kituoni hapo Jijini Dar es Salaam huku akieleza takribani simu 40,000 zinapokelewa lakini lakini ni 12,000 pekee ndio zinasikilizwa na kuongeza kuwa kitengo cha huduma kwa wateja kinatakiwa kuja na mikakati ya muda mfupi, ili kuhakikisha wateja wote wanasikilizwa na changamoto zao kupokelewa..
“Kuna upungufu kadhaa simu zinazopigwa hapa ni 40,000 lakini zinazopokelewa ni 12,000 kwa siku hii inatufikirisha kwa ajili ya namna bora ya kuboresha huduma na kuhakikisha watanzania wote wanaopiga simu wanapata huduma” amesema Kapinga.
Amesema, ni jambo lisilovumilika kwa Shirika lililo na zaidi ya miaka 50 kuzungumzia changamoto ya huduma kwa wateja huku wakieleza wanafahamu kuna changamoto sugu ndani ya TANESCO huku akitaka zitafutiwe ufumbuzi.
“Tulipofikia umeme si anasa bali ni jambo la msingi kwa mtanzania, huwezi kumuacha mteja akae saa 12 kwasababu umeshindwa kwenda kumtatulia tatizo lake mgao ni kitu kingine na kumtatulia mtu changamoto kwa wakati ni jambo lingie” amesema Kapinga.
Hata hivyo, amewataka kuacha kusingizia mvua kuwa sababu ya kukosekana huduma kwa wakati kwani ilikuwa ni lazima wajipange kwa kubadilisha miundombinu huku Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja, Martine Mwambene akisema moja ya mambo yatakayofanyiwa kazi kwa haraka ni njia mbadala ya kuripoti matatizo yao.