Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewezesha fani ya Uhasibu nchini kwa kudhamini kongamano la tatu la wanawake wahasibu Tanzania (TAWCA).
Akizungumza katika kongamano hilo jijini Arusha, afisa mkuu wa fedha wa TANESCO, CPA Renata Ndege, amesema TANESCO inatambua umuhimu wa fani ya Uhasibu kwani imekua sehemu ya kuwezesha ukuaji wa shirika hilo haswa katika kuhakikisha mahesabu yanafanyika vizuri na mikakati ya TANESCO inaendelea .
“TANESCO imedhamini kongamano hili la wanawake wahasibu Tanzania kama sehemu ya kusaidia na kushirikiana na jamii kwa kufahamu umuhimu wa kuwezesha fani ya Uhasibu, TANESCO imekua mfano mzuri wa kuwa na wahasibu wanawake wengi ambao wamekuwa chachu ya maendeleo ya Shirika” amesema CPA Renata.
Aidha, Renata, amewataka wanawake wahasibu ambao ni viongozi katika sekta mbalimbali nchini, kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na bidii ili kuleta maendeleo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Naye balozi Liberata Mulamula aliyehudhuria kama mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisema amefurahishwa kuona viongozi wakubwa wa Taasisi mbalimbali nchini katika fani ya uhasibu ni wanawake na taasisi hizo zimekua zikifanya vizuri kiutendaji.
“Nimefurahi kujua kuwa mhasibu mkuu wa fedha wa TANESCO ni mwanamama, SGR pia ni mwanamama. Taasisi nyingi hapa viongozi wao katika uhasibu ni wakinamama na kinamama tunaweza, kama mnayvoona TANESCO inaendelea vizuri sote tunapata umeme lakini moja wapo ya kiongozi pale ni mwanamke Mhasibu”, amesema Balozi Liberata.