Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Angola, zimesaini Hati mbili za Makubaliano (MoU), kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC), na Ushirikiano kati ya Chuo cha Diplomasia cha Tanzania (CFR), na Chuo cha Venancio de Moura cha Angola.
Makubaliano hayo, yamesainiwa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Balozi Téte António katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Mara baada ya kusaini Hati hizo za Makubaliano, Dkt. Tax alisema Tanzania na Angola zimekuwa zikishirikiana kwa muda mrefu, na Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuzisaidia nchi za Kusini mwa Bara la Afrika kujikomboa na tangu wakati huo imeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali.
“Leo tumeona ni vyema turasimishe ushirikiano wetu kwa sababu dunia inakwenda mbele na kuna mambo mengi ya kufanya pamoja na hivyo tumesaini Hati mbili za Makubaliano ya kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja itakayotuwezesha kukutana na kujadili masuala mbalimbali yenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema Dkt. Tax.
Kuhusu Makubaliano ya Ushirikiano wa Vyuo vya Diplomasia kati ya Tanzania na Angola, Waziri Tax alisema kupitia makubaliano hayo vyuo hivyo vitaweza kubadilishana uzoefu, utaalamu na wanafunzi ili kuboresha taasisi hizo za diplomasia.
Kwa Upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Angola, Balozi Téte António amesema Angola imefurahishwa na uamuzi wa Serikali ya Tanzania kukubali kuanzisha Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) na kuelezea utayari wake wa kushirikiana katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Tanzania na Angola ni marafiki wa siku nyingi, kupiti makubaliano tuliyosaini leo tumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya mataifa yetu, tunayo mengi ya kushirikiana,” alisema António.
Hata hivyo amesema, “waangola tumekuwa tukija kujifunza masuala mbalimbali ya kidiplomasia katika Chuo cha Diplomasia (CFR) na kuwa wanadiplomasia, hivyo kupitia makubaliano ya leo tutaweza kubadilishana uzoefu wa kidiplomasia na kuwanoa wanadiplomasia wengi zaidi.”