Serikali nchini, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuweka mikakati madhubuti katika masuala ya menejimenti ya maafa, ili kuhakikisha inapunguza madhara yatokanayo na maafa.

Kauli hiyo, imetolea na Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja Jenerali Charles Mbuge wakati akifungua kikao kazi cha wadau cha kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura, kilichofanyika Februari 16, 2023 Jijini Dodoma.

Amesema, upo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa dharura.

“Hakikisheni kuwa mpango unazingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022, Kanuni za Usimamizi wa Maafa za mwaka 2022 na Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wakati wa Maafa 2022 ili kurahisisha utekelezaji wake,” alisisitiza Meja Jenerali Mbuge.

Aidha, ameongeza kuwa mpango huo uliojikita kidijiti utarahisisha mawasilino ya haraka, sahihi na kwa wakati unaohitajika kwa kuzingatia mfumo na unahusisha vyombo vya habari ikiwemo matumizi ya radio, televisheni na mitandao ya kijamii.

Meja Mbuge amesema, “juhudi hizi zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na Wizara, Taasisi, Mashirika ya kimataifa na Asasi zisizo za kiserikali na Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya Mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Na. 6 ya mwaka 2022 inajukumu la kuratibu na kusimamia masuala ya maafa nchini.”

Idara ya maafa ilizindua nyaraka za usImamizi wa maafa nchini, ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ya Dharura 2022 ambao umelenga kuhakikisha utendaji kazi, ushirikiano, na mwendelezo wa mawasiliano vinaimarika wakati wa maafa ili kuruhusu watoa huduma za dharura kufanya mawasiliano baina yao na ngazi nyingine za serikali wakati wote, hata pindi miundombinu ya mawasiliano itakapoharibiwa.

Kikao kazi hicho kililenga kupitia na kujadili rasimu ya mpango huo wenye malengo ya  kusimamia mawasiliano na kuweka utaratibu wa matumizi ya huduma za mawasiliano ndani ya Serikali, Umma, Wadau wa Mawasiliano na Mashirika Binafsi.

Tanzania, Angola wasaini makubaliano tume ya kudumu
Dkt. Kimei: Wapinzani msipinge kila kitu, CCM haina ubaguzi