Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefungua Kongamano la Tano na Maonesho ya Nishati Tanzania na kusema Serikali imedhamiria kuwa mzalishaji mkubwa na Nishati kwani Tanzania haitegemei kuzalisha umeme kwa kutumia maji pekee bali inaweka mkazo wa uzalishaji wa vyanzo vingine ikiwemo gesi na jua..
Majaliwa ameyasema hayo leo Septemba 20, 2023 baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili linalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam na kuidai kuwa nishati ni sekta muhimu katika kufikia lengo la uanzishwaji wa viwanda ili kuimarisha shughuli za kiuchumi.
Amesema, “tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada tutauza nje ya nchi. Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili kufungua fursa kwa Watanzania wote.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha umeme unapatikana wakati wote nchini na kwamba zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki.
Amesema, ili kuwaendeleza Wafanyabiashara wa ndani na Watanzania kushiriki katika sekta ya nishati, Serikali itaendelea kuhakikisha kanuni na taratibu zinazofaa zinawekwa ili kuwezesha ushirikishwaji katika mnyororo wa thamani wa maendeleo kwenye sekta ya nishati.
Kongamano hilo la Kimataifa la Nishati, ambalo limehusisha Viongozi na Wadau kutoka Mataifa mbalimbali Duniani litajadili namna bora ya kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa nishati, huku akitumia fursa hiyo kuzisisitiza nchi wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo sekta za nishati.