Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uganda zimetia saini mkataba mahsusi utakaowezesha kuanza kwa kazi ya upembuzi yakinifu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi kutoka Tanzania kwenda Uganda.
Mkataba huo umesainiwa leo jijini Dodoma na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt. Doto Biteko pamoja na Mhe. Ruth Nankabirwa, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri ya Uganda.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, kusainiwa kwa Mkataba huo kumetokana na Makubaliano ya Awali (Memorandum of Understanding – MoU) kati ya nchi hizi mbili yaliyosainiwa mwezi Agosti, mwaka 2018 kwa ajili ya ujenzi wa Bomba la kusafirisha Gesi Asilia kutoka Tanzania kwenda Uganda kutokana na Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi katika kina kirefu cha bahari na nchi kavu.
“ Nchi hizi mbili zimekubaliana kufanya kazi ya upembuzi yakinifu kwa pamoja kuwezesha tathmini ya mradi na kutoa muongozo wa uwezekano wa mradi ikiwemo muundo wa mradi, mahitaji ya gesi, ukubwa wa bomba na taarifa nyingine muhimu zinazohusu mradi huo kwa ajili ya kufanya maamuzi.” Amesema Dkt. Doto Biteko
Dkt. Biteko amesema kuwa, Nishati ni ufunguo wa maendeleo kwa nchi yoyote ile duniani na umoja ni nguvu hivyo ametoa wito kwa nchi hizi mbili kutumia fursa ya kutekeleza mradi huu ambao utaunganisha nchi hizi mbili katika nyanja ya kiuchumi na kijamii.
Amesema kuwa, licha ya Tanzania kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilia takiriban futi za ujazo trilioni 57.54, mahitaji ya rasilimali hii yanakua kwa kasi ndani na nje ya nchi na hii inapelekea Serikali kuweka nguvu zaidi katika utafutaji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Eyasi Wembere, Mnazi Bay Kaskazini, Songosongo Magharibi, Ziwa Tanganyika na katika kina kirefu cha maji baharini.
Ameongeza kuwa, Tanzania inaendelea kutafuta wabia wa kimkakati watakaoweza kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ili kutafiti na kuendeleza vyanzo vya upatikanaji wa mafuta na gesi.
Pamoja na kupongeza timu zilizofanya kazi hadi kupelekea kusainiwa kwa mkataba huo, ameagiza kuwa kazi zilizopangwa kufanyika baada ya kusainiwa kwa mkataba huo zifanyike kwa wakati ikiwemo upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi wa kufanya kazi hii na kila upande unapaswa kuona kuwa mradi huo ni wa kipaumbele.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini kutoka nchini Uganda Mhe. Ruth Nankabirwa amesema kuwa, Uganda inatambua umuhimu wa mradi huu na kuongeza kuwa kumekuwepo na mahitaji makubwa ya matumizi ya gesi hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha kunakuwepo na uharakishwaji wa mradi huo.
Ameitaka Kamati ya pamoja ya utekelezaji wa Mradi huo kuhakikisha wanaharakisha mchakato wa manunuzi ya Mshauri Mwelekezi wa mradi ili kuharakisha upembuzi yakinifu tayari kwa utekelezaji.
Aidha, amesema Tanzania na Uganda zimekuwa zikishirikiana katika miradi mbalimbali kwenye Sekta ya Nishati ikiwemo Mradi wa uzalishaji wa umeme wa maji Megawati 14 wa Kikagati, mradi wa kusafirisha umeme kutoka Masaka Mutukula hadi Mwanza na mradi wa Bomba la Mafuta ambalo waliona lipite Tanzania.
Hafla hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makatibu Wakuu wa Wizara za Nishati kutoka nchi zote mbili, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Balozi wa Uganda nchini Tanzania, Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hizo ikiwemo TPDC, EWURA, PURA na UNOC na wawakilishi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.