Takribani watu wanane huambukizwa Virusi vya Ukimwi (VVU) kila baada ya saa moja nchini Tanzania, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko amesema takribani watu 72,000 hupata maambukizi ya VVU kila mwaka.
“Watu 72,000 huambukizwa Virusi Vya Ukimwi kila mwaka. Hii ni sawa na watu 6,000 kila mwezi, au watu 200 kila siku au watu wanane kila baada ya saa moja,” amesema Mwaluko.
Amefafanua kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 40 ya maambukizi yote nchini, hali inayofanya kundi hilo kuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi mapya.
Serikali imepanga kufanya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yenye kauli mbiu ya ‘Tuwajibike kwa Pamoja’, kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 1, 2020 mkoani Kilimanjaro.
Mgeni rasmi kwenye siku ya kilele cha maadhimisho hayo kwa mujibu wa Mwaluko atakuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.