Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeihibitishia jumuiya ya kimataifa kuwa itaendelea kutoa vikosi vya kulinda amani na ulinzi katika nchi za bara la Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati alipokuwa katika mkutano wa kunzindua kikosi kazi cha kuandaa mpango kazi wa kitaifa juu ya wanawake, amani na usalama jijini Dar es Salaam.

“Tanzania imekuwa ni nchi mojawapo inayotoa askari wanaokwenda kulinda amani katika mataifa mbalimbali katika bara la Afrika ambapo baadhi yake ni Sudani, Congo DRC, Lebanon na Afrika ya kati kwa hiyo lengo la mpango kazi huu ni kuwezasha Serikali ya Tanzania kuboresha ushiriki wa askari wa kike katika masuala ya ulinzi na amani,” Amesema Prof. kabudi

Aidha, ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kutoa askari wa kulinda amani katika mataifa mbalimbali barani afrika kwani suala la amani katika jamii ni jambo muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa lolote lile Duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema kuwa Taasisi anayoiongoza iko tayari kufanya kazi kwa karibu na jumuiya ya kimataifa na washirika wote wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa amani na utu wa mwanamke unalindwa na kuheshimiwa katika jamii.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo pia ulihudhuriwa na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, akiwemo Balozi wa Norway, Mhe. Elisabeth Jacobsen, Balozi wa Nchi za Falme za Kiarabu, Khalifa Ali-Marzouki, Balozi wa Canada Pamela O’Donnell pamoja Mratibu Mkazi wa Shughuli za Umoja wa Mataifa (UN) Zlatan Milišić.

 

Tanzania yapata cheo Umoja wa Mataifa
Uganda: Vyombo vya habari vyasusia agizo la museveni