Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Wilmar International Kuok Khoon Hong leo Juni 18, 2021 Ikulu jijini Dar es salaam ambapo kampuni hiyo ipo tayari kupanua uwekezaji wake katika uzalishaji kilimo nchini.
Rais Samia amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kampuni hiyo katika uwekezaji huo na ameagiza wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango kuandaa andiko la pamoja na kampuni hiyo litakalowezesha ushirikiano huo
Mwenyekiti Hong amesema kuwa kampuni hiyo ipo tayari kupanua uwekezaji wake katika uzalishaji wa mchele na mafuta hapa nchini, kwa kuwa mchele wa Tanzania ni bora na una soko kubwa duniani na mahitaji ya mafuta ni makubwa ndani ya nchi.
Kampuni hiyo yenye makazi yake nchini Singapore imewekeza dola milioni 150 za Kimarekani katika kiwanda cha kusafisha mafuta ya kupikia, kutengeneza sabuni pamoja na tambi ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa takribani dola bilioni moja za Kimarekani Barani Afrika.
Aidha Kwa sasa kampuni ya Wilmar imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kukoboa mpunga na kufungasha mchele mkoani Morogoro, kitakachokuwa na uwezo wa kukoboa tani 300 za mpunga kwa siku na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 300.