Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Wilson Mahera ametangaza tarehe ya uchaguzi mdogo katika jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga lililokuwa likiongozwa na aliyekuwa Waziri wa ulinzi Jeshi la kujenga Taifa Elias John Kwandikwa.
Akizungumza na vyombo vya Habari leo Ijumaa Agosti 27, Dkt. Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Yenye kumb. Na. CEA. 137/400/02/111 ya Tarehe 16 Agosti 2021, akiitaarifu kuhusu kuwepo kwa nafasi wazi ya ubunge Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga.
Nafasi hiyo ni baada ya kifo cha aliyekuwa Mbuge wa Jimbo hilo Elias John Kwandikwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Dkt. Mahera amesema taarifa hiyo ya spika ni kwa mujibu wa kifungu cha 37(3) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343.
Aidha Dkt. Mahera amesema kampeni za uchaguzi huo zitaanza Septemba 20, 2021 na zitafika ukomo wake Oktoba 8,2021 na uchaguzi kufanyika Oktoba 9 mwaka huu.
Dkt. Mahera amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi, taratibu, miongozo na maelekezo yatatolewa na Tume katika kipindi cha uchaguzi mdogo.