Serikali imewaagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara mjini na Vijijini – TARURA Mikoa na Wilaya zote nchini, zinazotekeleza mradi wa kuboresha Miundombinu katika Majiji, Manispaa na Miji (TACTIC), kusimamia hatua zote za manunuzi na kuhakikisha Wakandarasi wanaanza utekelezaji wa miradi hiyo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange hii leo Septemba 4, 2023 Bugeni jij8ni Dodoma, wakati akijibu Swali la Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mrisho Gambo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Stendi ya Kisasa kwenye eneo la Bondeni City Jijini Arusha kupitia Mradi wa TACTIC.
Amesema, Serikali kupitia Mradi wa TACTIC itatekeleza ujenzi wa stendi kuu ya kisasa ya mabasi, Masoko mawili pamoja na Bustani moja ya mapumziko kwenye eneo la Bondeni City, kwa lengo la kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa Wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani.
Aidha, Dkt. Dugange pia ameeleza kuwa katika utekelezaji wa mradi wa TACTIC, tayari kazi ya usanifu imekamilika na taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata mzabuni inatarajiwa kufikiwa Desemba 2023, baada ya taratibu husika kutekelezwa na ujenzi kwenye maeneo yaliyoainishwa kutarajiwa kuanza.