Shirika la viwango Tanzania TBS, limeanza kufanya ukaguzi wa magari unafanyika baada ya magari yaliyotumika kuingia nchini , ambapo hapo awali ukaguzi huo ulikuwa ukifanyika nje ya nchi na mawakala waliokuwa wanafanya kwa niaba ya TBS.
Akizungumza na Dar24 Media, Meneja wa ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje, Mhandisi Said Issa Mkwawa amesema kuwa katika ukaguzi huo gari ambalo halikidhi vigezo halipewi cheti na kumuagiza mwenye gari kulipeleka ‘garage’ (karakana) yoyote nchini anayoiamini na kukirudisha tena kukaguliwa katika moja ya kituo cha ukaguzi huo cha UDA.
Amesema kuwa katika ukaguzi huo matatizo waliyobaini ni pamoja na matatizo ya magurudumu, taa na mengineyo ambapo ni matatizo madogo ambayo yanaweza kutatuliwa katika karakana ndani ya nchi.
Mhandisi Mkwawa amesema kuwa kuna mashine za kisasa zinazofanya ukaguzi wa magari, kila gari moja lina uwezo wa kukaguliwa ndani ya dakika kumi na tano na kwa moja magari manne ambapo ukaguzi huo unafanyika masaa 24 katika vituo vya ukaguzi huo.
Aidha, Mhandisi Mkwawa amesema zoezi la ukaguzi toka lilipoanza nchini limekuwa na mafanikio makubwa kwa upande wa mapato ya serikali kwa kuiingizia serikali kiasi cha shilingi Bilioni 1.9.
“Hapo awali wakati ukaguzi unafanyika nje ya nchi tulikuwa tukipata serikali asilimia 30ya mapato ambayo katika bilioni moja ingekuwa ni kiasi cha kiwango cha milioni 576lakini timefanya ukaguzi huu nchini tumeweza kuokoa billioni 1.9 haya ni mafanikio kwa serikali yetu,” amesema Mkwawa.
Mpaka kufikia sasa TBS imefanya ukaguzi wa magari 5445.