Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lina jumla ya maabara tisa ambazo zinatumika katika uchunguzi wa bidhaa mbalimbali ambazo ni bora na kuna vifaa vya kisasa vya uchunguzi pamoja na wataalamu waliobobea katika uchunguzi.
Ameyasema hayo Meneja wa Upimaji (TBS), Joseph Makene wakati akitoa taarifa juu ya ufanyaji kazi wa maabara hizo zilizopo Makao Makuu ya Shirika hilo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makene amesema TBS ina maabara za kupima nguo na ngozi, maabara hizo zinatumika katika uchunguzi wa bidhaa zote zinazohusu nguo na ngozi pia kuna maabara za kupima vifaa vya kikemikali ambayo hutumika kupima vipodozi pamoja na bidhaa zote za petroli.
Aidha Makene amesema TBS ina maabara tatu za uhandisi ambapo kuna maabara ya uhandisi umeme ambayo inafanya uchunguzi wa vifaa vyote ambavyo vinahusiana na umeme kama vile Tv,simu, kompyuta na vingine vingi.
Amesema kuna maabara ya uhandisi mitambo ambayo inafanya uchunguzi wa bidhaa zote zinazohusu mitambo.
Vilevile amesema kuna maabara ya Ujenzi inayopima bidhaa zote za ujenzi kama mabomba yanayotumika katika kupitisha maji majumbani na kwenye miradi mbalimbali.
Hata hivyo kuna maabara zingine ambazo ni maabara ya kupima vifungashio na maabara ya ugezi ambayo inafanya ugezi wa vipimo vyote ambavyo vinatumika katika uzalishaji viwandani pamoja na kwenye hospitali.