Teknolojia ya Habari na Mawasiliano – TEHAMA, imefanikiwa Kuanzisha mradi wa kujengwa kituo kikubwa cha Taifa cha Ubunifu Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa huduma kwa wataalam, watafiti, na wabunifu wa tasnia hiyo nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Dtk. Nkundwe Mwasaga amesema ipo miradi mbalimbali ambayo imefanikiwa kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 ikiwemo kituo cha ubunifu Zanzibar.
Amesema, “tumefanikiwa Kuanzisha kituo kimoja cha ubunifu TEHAMA Zanzibar, vinne vya Kanda katika majiji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Tanga, Lindi na Mbeya kwa ajili ya kuendeleza kampuni changa za TEHAMA na kuendeleza kituo cha Dar es Salaam ili kukuza kiwango cha uzalishaji wa bidhaa za TEHAMA na kukuza uchumi wa nchi.”
Dtk. Mwasaga wamesema wamefanikiwa kuwezesha mijadala miwili ya wadau kutoka sekta ya Umma na Binafsi inayohusu maboresho ya sheria katika sekta ya TEHAMA na kuvutia uwekezaji ili kuharakisha ukuaji wa sekta kwa kuihusisha sekta binafsi.
“Na Mijadala hiyo imeiwezesha Tume kusaini mikataba ya maelewano ya uwezeshaji katika TEHAMA na mashirikika na taasisi mbalimbali zikiwemo Benki ya CRDB, UNCDF, UNDP, DOT na UNESCO, pia tumetengeneza mfumo jumuishi utakaounganisha usajili na uendelezaji wa wataalam na wabunifu TEHAMA nchini,” amesema Dkt. Mwasaga.
Hata hivyo, amesema lengo la mfumo huo ni kutambua bunifu na kupanua wigo wa ukuzaji wa wabunifu na bidhaa na huduma za TEHAMA zinazozalishwa Tanzania na hivyo kukuza pato la Taifa na kuongeza fursa za ajira kupitia TEHAMA na maendeleo ya kidijitali duniani.