Tembo sita wameripotiwa kupoteza maisha wakiwa wanajaribu kuokoana katika maporomoko ya maji kwenye Hifadhi ya Taifa ya Khao Yai nchini Thailand.
Kwa mujibu wa BBC, maafisa wa hifadhi hiyo wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakieleza kuwa chanzo ni mtoto wa tembo aliyetereza na kuanguka kwenye eneo la maporomoko ya maji yanayofahamika kama ‘Haew Narok’.
Miili ya tembo wengine watano imekutwa karibu na maporomoko hayo, ikielezwa kuwa walianguka wakati wakijaribu kumuokoa mtoto huyo wa tembo.
Mkuu wa hidafhi hiyo, Khanchit Srinoppawan amesema kuwa tembo wengine wawili waliokuwa wakijaribu kujiokoa kwenye kingo ya maporomoko hayo waliokolewa.
Tembo hao wanaendelea kupatiwa matibabu na wamewekwa chini ya uangalizi maalum na Idara ya Hifadhi ya Taifa ya Thailand.