Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke – TRRH, imeanza kutoa huduma za kiuchunguzi kwa wahisiwa(Presumptive) wa kifua kikuu kupitia kipimo hicho kipya. Ambacho kinatumia Vinasaba (Stool for Gene xpert) na kufanikiwa kugundua wagonjwa kadhaa ikiwemo mtoto wa miezi 5.
Hayo, yamesemwa na Mtaalamu wa Kifua kikuu na Ukoma kutoka Hospitali hiyo, Dkt. Rose Chagama na kuongeza kuwa kipimo hicho ni kipya kwa Tanzania na kwa Temeke Hospitali na kwamba huduma ya kipimo cha Kifua kikuu kupitia Haja kubwa, ni kipimo mahususi kwa makundi maalumu.
“Kipimo hiki ni kwa wale wahisiwa (Presumptive) wa kifua kikuu, ambao wapo katika makundi maalamu kama vile watoto waliopo chini ya miaka mitano ambao hawawezi kutoa makohozi, wagonjwa waishio na Maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na wale walioumwa muda mrefu na wapo vitandani hawajiwezi,” amesema.
Aidha, Kupitia kipimo hicho itasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kupunguza vifo vya watoto waliopo chini ya miaka mitano na kwa wagonjwa waishio na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwani Kifua kikuu ni moja ya Magonjwa nyemelezi yanayowapata na wengi kupoteza maisha Dr. Chagama amesema.
Wizara ya Afya Nchini, inaendelea kuboresha afya za Wananchi kwa kuweka mazingira wezeshi ya kufanya tafiti mbalimbali zinazopelekea ugunduzi wa njia mbadala za kuimarisha Afya na kupunguza vifo Tanzania.