Meneja wa Manchester United Erik Ten Hag ameonesha kusikitishwa na kitendo cha kukosa uthabiti katika maamuzi ya waamuzi baada ya kuchoshwa na uchezeshaji wa mwamuzi Anthony Taylor kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England mwishoni mwa juma lililopita uliomalizika kwa suluhu dhidi ya Southampton.
United waliambulia sare hiyo kwenye Uwanja wao wa Old Trafford baada ya Casemiro kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja katika kipindi cha kwanza kutokana na Mbrazil huyo kumfanyia Faulo mbaya, Carlos Alcaraz.
Awali, mwamuzi Taylor alimwonyesha Casemiro kadi ya njano, lakini baada ya kupitia ukaguzi wa VAR akaifuta kadi hiyo na kumwonesha nyekundu ya moja kwa moja.
Ina maana Casemiro ndiye mchezaji wa kwanza wa United kupokea kadi mbili nyekundu katika msimu mmoja wa Ligi Kuu tangu Nemanja Vidic msimu wa 2013-14, na atatumikia adhabu ya kufungiwa michezo minne badala ya mitatu kwa sababu ni mara ya pili ndani ya msimu mmoja.
“Ninachofikiria ni kutokwenda sawa, wachezaji hawajui tena sera ni nini, na nadhani yote ni katika kila mashindano,” amesema Ten Hag akiwaambia waandishi wa habari.
“Tuliona kwenye mchezo wa Leicester na Chelsea hakukuwa na VAR, lakini kwetu ilikuwapo.”
“Tulipaswa kupata Penati, hasa ile ya kwanza kwani ilikuwa ya wazi na ya wazi ya mpira wa mikono, kwa hiyo sera ni nini?”
“Ni kweli, tunazungumza, lakini si mengi, kwa hiyo baadhi ya maswali bado tunayo,”
“Na ninakuambia: Casemiro ni mchezaji wa haki. Casemiro amecheza mechi zote za Ulaya, zaidi ya 500 hakuwahi kuwa na kadi nyekundu (ya moja kwa moja). Sasa ana mbili.
“Fikiria hilo. Anacheza, lakini anacheza kwa haki. Na pia katika hili, anacheza kwa haki, sawa na dhidi ya Crystal Palace, kwa hivyo inajadiliwa sana.”