Mshambuliaji kutoka DR Congo na Klabu ya Simba SC Jean Baleke, amekubali kumuachia Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele Tuzo ya Ufungaji Bora ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, huku yeye akipiga hesabu za kufikisha mabao kumi.

Baleke ametoa kauli hiyo baada ya kuiwezesha Simba SC kupata ushindi wa 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar iliyokuwa nyumbani Manungu Complex, mkoani Morogoro, akifunga mabao yote.

Nyota huyo mwenye mabao matano katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ni kati ya Wachezaji wapya waliosajiliwa Simba SC katika usajili wa Dirisha Dogo akitokea TP Mazembe ya DR Congo.

Baleke amesema ni ngumu kwake kumfikia Mayele katika mbio za kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora kutokana na idadi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyobaki.

Baleke amesema, kama angekuwepo tangu mwanzoni mwa msimu huu, basi angehakikisha anapambana na Mayele katika vita hiyo ya Ufungaji Bora.

Ameongeza kuwa hivi sasa kitu kikubwa atakachokifanya ni kuhakikisha anaifungia timu yake mabao yatakayowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi.

“Ngumu kwa sasa kutangaza kuwania ufungaji bora kutokana na idadi ya michezo iliyobaki, hivyo basi ninampa nafasi kubwa Mayele ya kuchukua ufungaji bora.”

“Ninaamini kama ningekuwepo tangu kuanza kwa msimu huu, basi ningeingia katika vita hiyo ya ufungaji. Nimepanga kufikisha mabao kumi msimu huu, kama nisipopata majeraha yatakayonisababishia nikae nje muda mrefu,” amesema Baleke.

Ikumbukwe kuwa, Mayele ndiye kinara wa mabao Ligi Kuu Bara msimu huu akifuga 15 hadi sasa, akifuatiwa na Moses Phiri na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ wote wa Simba ambao kila mmoja ana mabao Kumi.

Nyama ya Kasa yauwa watu saba Mafia
Ten Hag akasirishwa na maamuzi England