Kocha Mkuu wa Manchester United Erik ten Hag amesema timu yake ilistahili kichapo cha 4-0 dhidi ya Crystal Palace, katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliopigwa usiku wa kuamkia leo Jumanne (Mei 06).

Man Utd walipokea kisago hicho wakiwa katika Uwanja wa ugenini Selhurst Park kusini mwa jijini London, na kujikuta wakiwa katika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England wakisalia na alama 54.

Kupoteza dhidi ya Palace kinakuwa kipigo cha 13 kwenye ligi kwa timu hiyo yenye mafanikio ya kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu nchini England, msimu huu 2023/24.

Kocha huyo kutoka nchini Uholanzi amesema: “Kama Man Utd tunapaswa kufanya vizuri zaidi. Wachezaji waliokuwepo wanapaswa kufanya vizuri zaidi. Tulicheza tofauti na mipango yetu kwa hiyo tulistahili kupoteza.

“Hatuwezi kumtazama na kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja. Tunapaswa kuzingatia uchezaji wa timu yote, ninaamini makosa tumefanya sote na ndio maana tumepoteza uwanjani. Hii haikuwa sawa.

“Ninakiri hivi ili ifahamike tumepoteza kihalali na tulichukuwe hili kama somo kwetu, kuelekea mchezo unaofuata dhidi ya Arsenal, ambao tutacheza tukiwa nyumbani Old Trafford.

“Ninawashukuru sana kwa mashabiki wetu ambao wamekubali klujitoa kwa hali zote, lakini haukuwa usiku mzuri kwa timu yao. Mashabiki wamekuwa nasi katika hali ya furaha na huzuni, hivyo sina budi kuwashukuru sana. Wanatambua tunapita katika kipindi kigumu. Kwa hiyo tunahitaji kushikamana kwa hali zote”

Ten Hag alipoulizwa kuhusu mustakabali wake klabuni hapo, amejibu: “Sifikirii juu ya hili. Ninaiandaa timu kwa njia bora niwezavyo. Tuna matatizo mengi. Lengo pekee nililo nalo ni kufanya vizuri zaidi na timu yangu.

“Nafikiria tu juu ya kuifanya timu yangu kuwa bora.”

United wamebakiwa na mechi tatu za ligi kabla ya kumenyana na wapinzani wao Manchester City katika fainali ya Kombe la FA.

Doroth Semu: Kuwa mpinzani ni kuchagua fungu la changamoto
Arne Slot athibitisha kuajiriwa Liverpool FC