Mwamba wa mpira wa miguu Tanzania, Kocha na Mkufunzi wa makocha nchini, Joel Nkaya Bendera hatunaye.
Bendera – Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amefariki dunia jana Jumatano Desemba 6, 2017 kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Joel Nkaya Bendera – Naibu Waziri Mstafu, Mkuu wa Mkoa (mstaafu) wa Manyara, alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali hiyo ya Taifa ya Muhimbili jijini.
Familia ya Marehemu Bendera aliyepata kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 – Jimbo la Korogwe Mjini, imetangaza kuwa Bendera atapumzishwa kwenye nyumba ya milele Jumapili alasiri katika Kijiji cha Manundu, Korogwe mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, taratibu za mazishi zinafanyika leo Alhamisi Desemba 7, mwaka huu na kesho Ijumaa kabla ya kuagwa Jumamosi Desemba 9, mwaka huu kuanzia saa 4.00 (1000h) asubuhi kwenye Viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Lugalo, Dar es Salaam.
Kaka wa marehemu, Michael Bendera amethibitisha kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Michael Bendera ametoa taarifa TFF kwamba Joel Bendera kwa muda mrefu alikuwa ana ugonjwa wa shinikizo la damu pamoja na kisukari japo ilikuwa nadra kufahamu kutokana na ukakamavu wake.
“Alishikwa na presha Jumatatu akiwa Korogwe. Jumanne wakaanza safari ya kuja Muhimbili. Alipofika Bagamoyo alizidiwa. Ikabidi apatiwe huduma ya kwanza, akapata nafuu na uongozi wa Hospitali ukatoa Ambulance (Gari la Wagonjwa), kuja huku Muhimbili),” amesema.
Amesema kwamba Muhimbili alikuwa akihudumiwa na madaktari mahsusi wa magonjwa hayo ambako hata hivyo jitihada hazikuzaa matunda kwa bahati mbaya akafariki dunia akipatiwa matibabu.
Michael Bendera ambaye alitoa shukrani kwa madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Bagamoyo na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema: “Ni kazi ya Mungu.”
Rais wa TFF, Wallace Karia ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la TFF, Mheshimiwa Mohammed Abdulaziz kutokana na kifo hicho.
“Sikuamini kwa mara ya kwanza nilipopigiwa simu na Mkurugenzi wa Ufundi, Mzee Madadi akinitaarifu kuhusu kifo cha Bendera. Nilihuzunika sana hasa ikizingatiwa kuwa juzi tu nimeongea naye.
“Aliniambia: “Mdogo wangu Karia sasa nimestaafu. Sasa nitumie nikutengenezee Walimu. Wakati tunataka kuanza kufanyia kazi mipango hiyo, ndio naletewa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Bendera, hakika nimeumia sana,” amesema Karia.
“Bwana alitoa, na Bwana ametwa. Tunalihimidi jina lake. Lakini niwaombe tu wanafamilia ya mpira wa miguu, ndugu, jamaa na marafiki kuwa watu wa subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema.
Kwanini Joel Nkaya Bendera ni Mwamba wa soka?
Joel Nkaya Bendera ni mwamba kwani kwa mengi aliyoyafanya kwenye mpira wa miguu, rekodi yake haijavunjwa hadi sasa.
Ndiye kocha msaidizi wa timu ya soka ya Tanzania aliyeongoza Taifa Stars katika kuiondoa Zambia na Tanzania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Tanzania mwaka 1979.
Taifa Stars ilishinda bao 1-0 dhidi ya KK Eleven ya Zambia (sasa Chipolopolo) na kuifanya Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo mikubwa Afrika kwa upande wa timu za taifa iliyofanyika Nigeria.
Bao lilifungwa na Peter Tino, lakini Taifa Stars haijafuzu tena katika michuano hiyo.
Joel Bendera – ndiye aliyeiongoza Simba kushinda mabao 5-0 dhidi ya Mufulira Wondereres huko Zambia katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1979.
Ikumbukwe kwamba Simba ilifungwa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam.
Joel Bendera – ndiye aliyeiongoza Coastal Union ya Tanga kutwaa ubingwa wa Bara na kucheza michuano ya Afrika Mashariki na Kati na kuifikisha timu hiyo fainali. Wakati akifanya kazi na hayati Zacharia Kinanda.
Joel Bendera – akiwa Naibu Waziri Michezo, chini Waziri George Huruma Mkuchika ndiye aliyeihamaisha Taifa Stars kucheza vema hadi kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), mwaka 2009.