Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ limesema limepata funzo kutokana na matukio yaliyojitokeza kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Young Africans dhidi ya USM Algiers uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili (Mei 28).
Katika mchezo huo mashabiki walivunja mageti na kuingia bure uwanjani, huku mmoja wao akifa kutokana na msongamano mkubwa uwanjani hapo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi wakati akizungumzia athari zilizotokana na mchezo huo wa fainali ya kwanza ikiwemo kifo cha shabiki mmoja.
Amesema kuanzia mechi zijazo watakuwa wanafuatilia kwa karibu kwani tukio hilo limetoa fundisho na kuna somo wamelipata na kuahidi kurekebisha mapungufu.
Pia amesema kwa uwezo mkubwa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ na FIFA wanaiamini Tanzania na kwa umoja huo wa Kenya na Uganda Afrika Mashariki wanakwenda kupata kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
Katika mchezo huo wa Fainali ya kwanza Young Africans ilipoteza kwa mabao 2-1 na watarudiana tena Jumamosi (Juni 3) nchini Algéria kwenye Uwanja wa Julai 5.